FIFA wamtakia heri Malinzi

“Nakutakia wewe na kamati mpya ya Utendaji iliyochaguliwa kila la kheri, nguvu, na kila aina ya mafanikio kwa changamoto zilizo mbele yenu.’’ Rais wa Fifa Sepp Blatter. Blatter alisema ana uhakika na ufahamu wake na uwezo wake katika uongozi ni muhimu katika kuimarisha Ukiacha salamu za pongezi za rais wa Fifa, pia viongozi mbalimbali wamempongeza Malinzi.
Dar es Salaam. Rais mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameendelea kupokea salamu za pongezi baada ya kushinda wadhifa huo katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 27 mwaka huu.
Salamu nyingine zimetoka kwa Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Sepp Blatter ambapo amempongeza Malinzi kwa kuchaguliwa na kumtakia kila la kheri katika majukumu yake ya kuongoza mchezo huo nchini.
Blatter alisema ana uhakika na ufahamu wake na uwezo wake katika uongozi ni muhimu katika kuimarisha maendeleo ya mpira wa miguu nchini na kuongeza kuwa milango ya FIFA iko wazi wakati wowote anapotaka kujadili masuala yanayohusu mchezo huo.
“Nakutakia wewe na kamati mpya ya Utendaji iliyochaguliwa kila la kheri, nguvu, na kila aina ya mafanikio kwa changamoto zilizo mbele yenu,” alisema Rais Blatter katika salamu zake.
Malinzi amerithi mikoba ya Leodegar Tenga ambaye ameongoza taasisi hiyo kwa miaka minane baada ya kumbwaga mpinzani wake, Athuman Nyamlani katika uchaguzi huo uliokuwa unavuta hisia za watu wengi.
Malinzi alishinda kwa kupata kura 73 dhidi ya 52 za Nyamlani.
Tayari Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete na Rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), Issa Hayatou wamekuwa wa mwanzo kumpongeza Malinzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Kagera.
Mbali na Blatter, wengine waliomtumia Rais Malinzi salamu za pongezi ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF), Sam Nyamweya, Rais wa Heshima wa Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA), Lawrence Mulindwa, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Arumeru (ADFA), Peter Temu.
Malinzi ambaye anatarajia kuanza kazi rasmi ndani ya shirikisho hilo Jumatatu baada ya kukabidhiwa ofisi kesho Jumamosi tayari alitangaza mikakati yake mbali mbali ya kuhakikisha anaboresha shirikisho hilo ikiwa ni pamoja na kupitia mikataba mbali mbali ya wafanyakazi na udhamini kuwa ndio kitu cha kwanza atakachoanza nacho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni